Tuesday, April 17, 2018

Sizonje - Mrisho Mpoto ft Banana Zorro

Sizonje hii ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Sizonje ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Tulikaa barazani tukasikia kelele
Kelele toka ndani mtu anaruka dirishani
Sizonje karibu nyumbani kwetu
Uone maajabu ya nyumba yetu
Karibu sana Sizonje hii ndo nyumba yetu
Tulipoficha mundu za kupondea wezi
Kwani makaburi yaliofukuliwa lazima yazikwe upya
Nyumba hii Sizonje ina vyumba vinne
Vitatu havifunguki kimoja hakina mlango
Japo kuwa kina watu ndani na hawaongei Kiswahili
Wenyeji wanalala sebleni na walishazoea
Sizonje kule tulipotoka panaitwa jikoni
Huna haja ya kwenda kule kumejaa mafundi wa kupika
Sasa hivi wanakupikia wewe ili ule ulale
Ukiamka muongee nini hasa ujio na dhima ya safari yako
Wanashangaa mbona ghafla
Samahani sana mgeni
Wapishi wameniomba kwamba
Nikuulize tena kwa kukuomba kwamba
Eti unapenda vya mafuta au vya nazi
Wanataka kukuonyesha madoido katika mapishi yao Sizonje
Sizonje chumba hiki naomba usiingie
Ukimaliza nitakwambia kwanini
Kuna sauti inajirudia mara kwa mara
Na hapa mlangoni kulikuwa na picha mbili kubwa
Moja picha nyingine mchoro wa picha wa kwanza
Ninachokumbuka iliwahi kuandikwa ‘Usiyemtaka Kaja’
Hatukuwahi kuelewa maana yake
Labda kwa sababu ya ujio wako unaweza kutusaidia
Sizonje hii ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Sizonje hii ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Najua wimbo mbaya haufai kubembelezea mtoto
Na kamwe mtoto hawezi kuungua
Kwa kiazi kilichokuwa kwenye kiganja cha mama yake mzazi
Njoo huku uone Sizonje
Si unajua harufu ya uzazi haiishi mpaka mtoto akue
Sawa Sizonje huu hapa ni ua
Lile pale ni shimo la taka
Na kile pale ni choo
Kinachotutisha na kutuogopesha zaidi
Wanaoishi humu ndani hawajawahi kutupa taka
Wala kwenda chooni
Kama ukiwa makini
Kwa nje utasikia sauti za makundi ya watu
Wengi ni vijana wana bahasha za khaki mikononi
Kama hamtupi taka shimo hili mlichimba la nini
Lakini pia kwenye sauti zao Sizonje
Kuna watoto wazee na kina mama
Ukiunganisha sauti zao ndio unapata hizo kelele
Ninavyosikia ila sina uhakika
Waliambiwa kihistoria nyumba hii ni ya kwao
Na wana haki ya kutupa taka na kutumia choo hiki
Sasa njoo nikuonyeshe huku uchochoroni
Uone maajabu mengine ya nyumba hii
Sizonje ukiona tembo anaringa
Ujue mvua zinakaribia
Sizonje hii ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Sizonje ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu
Ingia uyaone maajabu ya nyumba yetu

No comments:

Post a Comment